Saturday 19 January 2013

VIJIMAMBO: Baraza la Maulamaa lazinduliwa Zanzibar

VIJIMAMBO
Baraza la Maulamaa lazinduliwa Zanzibar
Jan 20th 2013, 00:11


Waliokaa mbele kulia ni Sheikh Abdallah Talib, Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji, katikati Waziri wa Sheria na Katiba Abubakar Khamis Bakari, Mufti Mkuu Sheikh Saleh Omar Kaabi na Sheikh Habib Ali Kombo Kadhi Mstaafu.

Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Maulamaa visiwa vyetu hivi vimekumbwa na wimbi kubwa la mabadiliko ya baadhi ya waumin. Ni ukweli usiopingika kuwa wakati wetu umekuwa na wasemaji wengi sana wanaozungumzia mambo ya kiislamu tokea mambo ya USULI hadi ya FURUU mambo haya yote yanahitaji elimu ya kina na hekimu kubwa hali ya kuwa wao sio Ahli wa ilmu. Bahati mbaya kila msemaji hupata wasikilizaji, mashabiki na hata waenezaji na wenye kuyanusuru maneno hayo. Hali hii imeleta mtafaruki mkubwa baina yetu, ikazaa migongano na hatimae makundi yenye kupingana ambayo yameidhoofisha dini na jamii yetu. Ni kweli uislamu haukuweka tabaka la watu wadini na wasio wa dini, lakini pia haukuwacha mambo shaghala baghala. Mtume Muhammad (S.A.W) amesema "wanachuoni ndio warithi wa Mitume". Tunajua kuwa umoja wetu wa Kiislam na mshikamano wetu wa sasa unaaza kumong'onyoka.

HOTUBA YA UZINDUZI WA BARAZA LA PILI LA MAULAMAA, TAREHE
19/01/2013 ILIYOTOLEWA NA MHE. ABUBAKAR KHAMIS BAKARY,
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA KATIKA UKUMBI WA ZAMANI BARAZA LA WAWAKILISHI

Bismillah Rahman Rahym
Mhe. Mufti wa Zanzibar
Sheikh Saleh Omar Kaaby

Mhe. Kadhi Mkuu
Sheikh Khamis Haji

Mhe. Naibu Mufti
Sheikh Mahmoud Mussa

Mhe. Naibu Kadhi Mkuu
Sheikh Hassan Ngwali

Mhe. Kadhi Mkuu Mstaafu
Mzee Wetu Sheikh Habib Ali Kombo

Wahe. Masheikh, Maulamaa na wageni waalikwa


Assalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatu


Alhamdulillahi Wahdahu Lasharikalahu, waswalatu wasalamu ala Nabiyina Muhamad (S.A.W), amma baadau

Mheshimiwa Mufti, mtoto wa jongoo alipotaka kutembea alimuuliza mama yake aende vipi? Atangulize mguu upi mwanzo, lakini jibu alilolipata kwa mama yake ni kumwambia "nenda mwanangu nenda". Mheshimiwa Mufti na Waheshimiwa wazee wetu na masheikh wetu, na mimi nimewekwa katika mtihani huo huo. Sioni haja ya kutoa hotuba ya uzinduzi wa Baraza la Ulamaa mbele ya visima vya elimu ya dini yetu. Chochote nitachokisema basi si zaidi ya tone moja la chumvi ndani ya bahari ya elimu yetu ya dini. Naomba kwa Uradhi wenu mniruhusu niseme machache ambayo yatakuwa na kasoro nyingi mbele ya wazee mliobobea katika misingi ya dini. Nawaombeni radhi sana kwa hayo
HISTORIA YA ZANZIBAR NA UISLAM
Mapema tu, mnamo karne za nyuma watu wa kale kama vile Sumerians, Assyrians, Hindus, Egyptians na Waarabu wa Kusini walitembelea mwambao wa Afrika ya Mashariki ambapo walikutana na makabila ya kienyeji kama vile Wahadimu, Wapemba na Watumbatu. Waarabu hawa, hasa kutoka Ghuba ya Uajemi (Persion Gulf) ndio walioanza kuuleta uislam na Wazanzibari wakaikubali kwa dhati dini hii.
Wanahistoria wengi wanaamini kuwa Uislam umeingia mapema kabisa katika mwambao wa Afrika ya Mashariki. Wakati mwanahistoria maarufu wa Moroko Ibun Battuta alipotembelea eneo hili alikuta wakazi wake ni waislamu na kiarabu ndio lugha ya fasihi kwa biashara.
Mnamo mwaka 1503 Zanzibar ilikaliwa na Wareno lakini katika karne ya 17 kulikuwa na ghasia katika mwambao huu ikiwemo Pemba. Mwaka 1652 Waarabu waliivamia Zanzibar na waliiteka Mombasa, Pemba na Kilwa mnamo mwaka 1698 na 1699. Visiwa vyote vikawa chini ya Imam wa Muscat Seyyid Said bin Sultan, Mwanzilishi wa Zanzibar na zao la karafuu. Yeye ndie aliyekuwa kiongozi. Mnamo mwaka 1804 akauhamisha mji mkuu wa Oman kutoka Muscat kuja Zanzibar na katika mwaka 1832, Zanzibar sasa ilijulikana kisiasa, kibiashara na kidini. Mbali na mabadiliko ya kiutawala kuanzia mwaka 1861, 1869 na 1872 lakini ilipofika mwaka 1891 Zanzibar ilikuwa na utaratibu wake kamili wa Serikali na Sir Lioyd Mathews ndiye aliyekuwa Waziri wa Kwanza (First Minister) na mweka hazina (Treasurer).
Muhimu hapa ni kuona kwamba Zanzibar imekuwa na Dini ya Kiislam kwa karne nyingi sana na sasa kila mtu anajua kwamba Uislam Zanzibar si dini tu peke yake lakini imechimba zaidi hata katika "culture", tabia, silka na hulka zetu. Waislam hapa Zanzibar ni zaidi ya asilimia 98% na tumeungana zaidi kwa lugha yetu moja na kuwa sote ni wamoja. Wajibu wetu wa kwanza wa Baraza hili ni kuunganisha umoja wetu huu kwa misingi nilioielezea hapo juu.
SHERIA YA MUFTI
Sheria ya Mufti, Na. 9/2001 inaanzisha Afisi ya Mufti pamoja na maafisa wengine wa Afisi hiyo. Kazi za Mufti zimeelezwa vyema katika kifungu cha 9(1) ikiwa ni pamoja na kutoa "fat-wa" ambapo katika kutekeleza kazi hii anaweza akashauriana na Ulamaa wa Zanzibar. Kifungu cha 15(1) cha sheria hiyo kimempa uwezo Waziri muhusika kufanya kanuni. Chini ya uwezo huo kwa tangazo maalum la Serikali Na. 52/2011 kumeanzishwa Kanuni za Baraza la Ulamaa ambapo chini ya kanuni ya 3 itakuwa ni chombo cha ushauri na kitajulikana kama ni Baraza la Ulamaa. Baraza hilo litaongozwa na Mufti atayekuwa Mwenyekiti na Wajumbe wafuatao:-
  1. Sheikh mmoja kwa kila Wilaya atayeteuliwa na Waziri kwa kushauriana na Mufti.
  1. Masheikh wanne (4) kutokana na ujuzi wao pia watateuliwa na Waziri baada ya kupata mapendekezo ya majina yasiyopungua sita (6) kutoka kwa Mufti.
  1. Naibu Mufti, Kadhi Mkuu, Naibu Kadhi Mkuu, Katibu Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na Mwalim Mkuu Chuo cha Kiislam ambao wao wanaingia kutokana na wadhifa wao.
Makatibu wa vikao hivi watakuwa Katibu wa Mufti na Msaidizi wa Katibu wa Mufti. Baraza hili kwa mujibu wa kanuni ya 5 linatakiwa likutane angalau mara mbili kwa mwaka na wanaweza kufanya kikao cha dharura pale inapohitajika. Mufti chini ya kanuni ya 5(2) anaweza kuunda kamati maalum itayoshughulikia tatizo lililojitokeza ila ni lazima atilie maanani suala zima la uwakilishi katika kamati hiyo, na kwamba maamuzi ya kamati hiyo yanaweza kukubaliwa, kutenguliwa au kufanyiwa marekebisho fulani katika kikao cha Baraza zima la Maulamaa.
KAZI ZENU
Wazee wetu, Masheikh na Maulamaa wetu, wajibu wenu na kazi zenu zipo chini ya kanuni ya 7 ya Kanuni za Baraza la Ulamaa ambayo inasema:
"Kazi ya Baraza ni kumshauri Mufti juu ya masuala ya
Kiislam yaliyowasilishwa kwake kwa kutolewa fat-wa
na kufanya kazi nyengine litakazopewa na Mufti".
Kazi zenu ni ngumu na zinahitaji uadilifu mkubwa, kujitolea, haki na ukweli. Ndio maana Imamu Ibnu Qaym amewaita wanachuoni kuwa ni watia saini (signatory) kwa niaba ya Mwenyezi Mungu. Sina wasi wasi hata chembe wa mambo haya juu yetu. Naamini na sote tunakubali kuwa Baraza limepata wajumbe wenye elimu, busara na hekma, waadilifu na wakweli; na hivyo basi msingi mkubwa wa mafanikio wa kazi zenu na wajibu wenu tunao. Haya sote tunayaelewa pale Mwenyezi Mungu alipotutanabahisha katika SuratulAl-Ahzab kwa kutukumbusha kuwa tutawakal kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi na kuwa sote tulioamini tumuogopeni Mwenyezi Mungu na tuseme maneno ya kweli.
Tunapoyafanya hayo kwa uadilifu, ukweli na haki kama ilivyo kawaida yenu, na tukavuta subra katika mitihani ambayo tutaipata wakati wa kutekeleza majukumu haya; basi Mwenyezi Mungu atazidi kuwa nasi. Mwenyezi Mungu mwenyewe anatukumbusha katika Qur-ani yake, katika Suratul Asr kuwaBinaadamu yuko katika hasara isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri na wakausiana kufuata haki na wakausiana kushikamana na subira (yaani) kustahamilianaJukumu hili nalo ni kubwa na ni zito lakini ndio wajibu wetu, na ni lazima kulifanya. Tukilifanya kwa misingi tuliyoielezea hapo juu basi nasi tutakuwa katika kundi la wataokuwa na kheri, Inshaalla Mwenyezi Mungu atujaalie kila la kheri, na kulitekeleza jukumu hilo zito kwa njia ile anayoipenda Mwenyezi Mungu. Ammin.
MABADILIKO YA TABIA YA BAADHI YA WAUMINI
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Maulamaa visiwa vyetu hivi vimekumbwa na wimbi kubwa la mabadiliko ya baadhi ya waumin. Ni ukweli usiopingika kuwa wakati wetu umekuwa na wasemaji wengi sana wanaozungumzia mambo ya kiislamu tokea mambo ya USULI hadi ya FURUU mambo haya yote yanahitaji elimu ya kina na hekimu kubwa hali ya kuwa wao sio Ahli wa ilmu. Bahati mbaya kila msemaji hupata wasikilizaji, mashabiki na hata waenezaji na wenye kuyanusuru maneno hayo. Hali hii imeleta mtafaruki mkubwa baina yetu, ikazaa migongano na hatimae makundi yenye kupingana ambayo yameidhoofisha dini na jamii yetu. Ni kweli uislamu haukuweka tabaka la watu wadini na wasio wa dini, lakini pia haukuwacha mambo shaghala baghala. Mtume Muhammad (S.A.W) amesema "wanachuoni ndio warithi wa Mitume". Tunajua kuwa umoja wetu wa Kiislam na mshikamano wetu wa sasa unaaza kumong'onyoka.
Kwa maana hiyo tujitahidini kufuata na kuhimizana maagizo ya Qur-ani:-

"Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi
Mungu nyote kwa pamoja na wala musifarikiane"
Hata katika hadithi tunatanabahishwa kwamba
"Hakika mfano wa Waislamu katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao na kurehemeana kwao ni sawa sawa na kiwiliwili kimoja''

Ni wajibu wenu mlio hapa, kuyajadili mambo kama haya na mengine zaidi ya haya ili mumshauri Mufti ipasavyo. Kamba hii ya Mwenyezi Mungu ambayo sasa waislam wanaanza kuihujumu inahitaji kulindwa isikatwe katwe. Nyinyi Baraza la Ulamaa ndio walinzi wetu. Roho zetu, macho, nafsi tamaa na kiu ya waislam wema zinawatazama nyinyi. Naamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mtafanikiwa kuielezea dini yetu kwa njia ya fat-wa na njia nyingi nyenginezo kwa kuielemisha jamii, kwa maslahi yetu na kizazi chetu na dini yetu.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kuwa kuna vyuo (maahad) vingi vinavyotoa elimu bora na vyuo hivyo vina walimu wazuri Unguja na Pemba. Hata hivyo kwa kukosekana umoja wa vyuo hivyo imekuwa tabu kwa mwanafunzi anaemaliza thanawi kujiunga na vyuo vikuu vyetu pamoja na kuwa vyuo vya nje wanakubaliwa. Natumai mtamshauri Mufti ili tuone namna gani tutaunganisha maahad zetu na kuwawezesha wanafunzi wake kunufaika na vyuo vikuu vyetu katika fani zao. Sadaka hazianzi nje bali kuanzia nyumbani.
UHURU WA DINI /KUABUDU NA HAKI ZA MTU
Bila shaka uislamu ni dini iliyotoa uhuru mkubwa kwa mwanaadamu kiasi cha Allah kukataza watu kulazimishwa kufuata dini. Uhuru ndio unaomtofautisha mwanadamu na malaika. Hata hivyo uhuru huo umeambatana na majukumu kwani hakuna uhuru usio na mipaka. Kikawaida uislamu unaangalia zaidi dhima (majukumu kuliko uhuru). Amesema Mtukufu,Subhanahu Wataala kuwa (na naapa) kwa nafsi na kwa aliyeitengeneza.Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wakeBila shaka amefaulualiyeitakasa (nafsi yake) na bila shaka amehasirikaaliyeiviza (Suratu Ash-Shams aya 7-10). Ili kujenga utawala wa sheria, haki na kulinda amani na utulivu nchi yetu inaamini dhana ya uhuru na haki za binadaamu. Kwa tafsiri iliyo rahisi ni kweli kifungu cha 18(1) na (2) cha Katiba kinachotowa uhuru wa maoni, kifungu cha 19(1), (2) na (3) kuhusu uhuru wa mtu kuamini dini atakayo na kifungu cha 20(1) kuhusu uhuru wa kujikusanya, vinaruhusu watu au waumini kufanya wanayotaka kwa kisingizio cha Katiba yetu ya Zanzibar.
Ni kweli vifungu vyote hivyo vinatoa uhuru wa muumini yeyote kufanya kile anachohisi ndani ya maoni yake. Lakini muumin huyo huyo anatakiwa asisome baadhi ya vifungu tu kwa maslahi yake, lakini avisome vifunguvyote vinavyohusiana na maudhui inayohusika. Sasa, kwa maana hiyo ukisoma vifungu vya Katiba vya 18, 19 na 20 ni lazima usome kwa pamoja na kifungu cha 23(1), (2), (3) na (4) pamoja na kifungu cha 24(1) kama vinavyojielezea hapo chini:
"23(1) Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na Sheria za Zanzibar, kuchukua hatua za kisheria kama zilivyowekwa, kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi.
(2) Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Zanzibar, mali ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuheshimu mali ya mtu mwengine.
(3) Watu wote watatakiwa na sheria kulinda vizuri mali ya Zanzibar na kwa pamoja kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa Zanzibar kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadae ya Taifa lao.
(4) Kila Mzanzibari ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi, kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa Zanzibar………."
"24(1) Haki na Uhuru wa binadamu ambayo misingi yake imeorodheshwa na Katiba hii haitatumiwa na mtu mmoja kwa namna ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma na inaweza kubanwa na sheriailiyotungwa na Baraza la Wawakilishi iwapo tu kibano hicho ni lazima na kinakubalika katika mfumo wa kidemokrasia…….."
Masheikh wetu, misingi hii ya Katiba naamini itawasaidia sana katika kazi zenu ambapo baadhi ya waumini hutumia vibaya uhuru wao na kusababisha fujo, kuingilia mali ya umma na kadhalika. Hivi sivyo na ni wajibu wetu sote na zaidi Baraza lenu tukufu kuwaelimisha sana waumini wa aina hii misingi mizuri ya dini, silka, tabia na khulka zetu za kiislam ambazo siku zote zinataka na zinasisitiza umoja, udugu na amani. Na sisi tunatakiwa kwanza tuitakie amani nchi yetu ya Zanzibar kama fundisho tulilopewa na baba yetu Ibrahim (AS) kwanza alipoiombea nchi yake amani na baadae akaiombea iwe na riziki na baraka. Kazi kubwa tunayo na hiyo ni changamoto kwenu, na ndilo jukumu lenu na wajibu wenu mwengine. Inshaalla Mwenyezi Mungu atawasaidia. Ammin.
MWISHO
Ninafahamu kuwa Baraza hili la Ulamaa lililopo mbele yangu ni la pili. Baraza lililopita ambalo lilikuwa chini ya Mufti aliyepita Almarhum Sheikh Harith Bin Khelef bin Khamis, Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi amin – limemaliza muda wake. Napenda kuchukuwa fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwa niaba yangu binafsi kuwashukuru sana sana wajumbe wa Baraza hilo na kuwatakia kila la kheri katika maisha yao. Napenda pia niwaombee malazi mema peponi wale wajumbe wetu wengine waliotangulia mbele ya haki wakiwemo Sheikh Mussa Makungu, Sheikh Ali Khatib Mranzi, Sheikh Abdulrazak Othman Juma, Sheikh Ali Mwinyi Kombo (Wilaya ya Kati) na Sheikh Suleiman Haji (Wilaya ya Mjini) na Sheikh Simai Daima ambao juhudi zao wakati wa uhai wao na hususan walipokuwa wakilitumikia Baraza lililopita zilionekana vizuri sana.
Pia nawashukruru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna wa Polisi na Mkuu wa Usalama ambao na wao kwa nafasi zao walikuwa ni wajumbe wa kualikwa kutokana na hali ya mivutano mingi ya kidini iliyokuwepo wakati huo. Wazee wetu kwa uelewa wao wanatuambia:
"paukwa pakawa'
yaani penye kuondokwa hukaliwa. Ninafuraha kusema Baraza la Ulamaa la kwanza limemaliza muda wake na limeshaondoka ingawa bado wamo wajumbe amabo wanaendelea baadhi yao wakiwa wameingia njiani na wengine wameingia mwanzo. Natumai uzoefu wao utawasaidia sana wajumbe wapya. Nyinyi mliopo hapa sasa mnajaza pengo lililowachwa wazi na wao. Sina wasi wasi hata chembe kwamba pengo hilo limejazwa vizuri na halina mwanya, ninawaombeni muendeleze zaidi kazi hizi za Baraza ili Zanzibar irejee kama enzi za zamani kwa kutambulika kuwa ndio chimbuko la dini yetu kwa Afrika ya Mashariki, Kati na Kusini. Nwakumbusha hadithi isemayo "Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwakuhusu kile mnachokichunga". Inshaalla, Mwenyezi Mungu atuwafikishie, natuwe wachunga wema. Ammin.
Baada ya maelezo hayo mafupi sasa natamka rasmi kuwa BARAZA LA ULAMAA LA PILI sasa LINAZINDULIWA RASMI
Wabillahi tawfik
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment