Friday 18 January 2013

VIJIMAMBO: SI KILA MPENZI NI WA KUVUMILIWA, WENGINE WAACHE WAPITE!

VIJIMAMBO
thumbnail SI KILA MPENZI NI WA KUVUMILIWA, WENGINE WAACHE WAPITE!
Jan 18th 2013, 23:01

KATIKA lugha ya Kiswahili kuna misemo mingi inayotoa muongozo wa namna tunavyoweza kuyaendesha maisha yetu. Ipo misemo ambayo unaweza kudhani inapotosha lakini mingi inagusa ukweli kwa namna moja ama nyingine.

Kuna huu msemo usemao, mvumilivu hula mbivu. Hakuna asiyejua elimu tunayoipata kutokana na msemo huu. Hakika siku zote mvumilivu mwishowe hula mbivu.
Kuthibitisha hili, wapo waliokuwa na uchu wa kufanikiwa lakini kwa kuwa muda wao ulikuwa bado, walijikuta wakiishi maisha yasiyotamanika. Baada ya kuvumilia leo hii wanayafurahia maisha yao.
Hili lipo hata katika maisha yetu ya kimapenzi. Uvumilivu una nafasi kubwa sana kiasi kwamba usipokuwa na subira, unaweza kukosa furaha ambayo Mungu amekupangia.

Umetokea kumpenda mtu fulani lakini kwa bahati mbaya ukakutana na tabia ambazo hukuzitarajia, unafanyaje katika mazingira haya? Je, ni sahihi kumuacha?
Hili haliwezi kuwa suala la kukuweka njia panda hata siku moja kama uelewa wako utakuwa mkubwa. Cha kufanya hapa ni kumvumilia na kumpa muda wa kubadilika.
Katika kipindi hicho, utajaribu kumueleza namna tabia zake zisivyokufurahisha. Kama kweli atakuwa anakupenda, nina imani atabadilika.

Umekutana na mwanaume mlevi kupindukia au mpenda totoz ukahisi ndiye mwanaume wa maisha yako, mpe muda! Kumpotezea yaweza kuwa ni kuipoteza bahati yako.
Kama huamini katika hili, jaribu kuchunguza na utabaini wengi ambao sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani walivumiliana kwa mengi hadi kufikia hatua uhusiano wao ukasimama. Kuwa na subira na wala usiwe mtu wa kukata tamaa haraka.
Katika maisha ya sasa, watu wamekuwa hawaeleweki, hakuna unayeweza kuwa na uhakika naye asilimia mia moja kuwa anakupenda kwa dhati, subira yako ndiyo itakufanya ugundue hilo.
Usichukulie eti kwa kuwa mara kwa mara unampigia simu hapokei basi ukadhani hakupendi. Kwa maisha ya sasa kumpima mtu katika hilo kunahitaji muda. Vumilia na siku uvumilivu ukikushinda, 'automatikale' utajikuta unajitoa. 

Mvumilie mpenzi wako huku ukijaribu mara kwa mara kuzungumza naye, usiwe mwepesi wa kuchukua uamuzi.
Hata hivyo, nitoe wito kwamba, tusiutumie vibaya msemo huo. Uvumilivu una kiwango chake. Usiwe wewe ni mtu wa kulizwa kila siku lakini unashindwa kuchukua uamuzi sahihi eti kwa kuwa tu umeambiwa mvumilivu hula mbivu. Vumilia lakini angalia usije ukala zilizooza badala ya zilizoiva.
Kumbuka si kila mpenzi unayekuwa naye anastahili kuvumiliwa kwa muda mrefu, wengine mapema kabisa wanaonekana hawafai hivyo ni uamuzi sahihi kuwaacha wapite.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
CHANZO: GPL

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment