Tuesday 25 December 2012

VIJIMAMBO: UHUSIANO BORA HUUNDWA NA MISINGI IMARA YENYE UKWELI

VIJIMAMBO
thumbnail UHUSIANO BORA HUUNDWA NA MISINGI IMARA YENYE UKWELI
Dec 25th 2012, 22:35

Makala haya yataiweka katiba hiyo kwenye maandishi kwa ajili ya kukusaidia msomaji wangu kujua jinsi ya kuishi ndani ya uhusiano wako. Wengi wamekuwa wakipata tabu, wanapotoka na kuishi nje ya mistari inayofaa kwa sababu hawajaisoma au hawaijui.
Unahitaji muongozo wa kikatiba ili mapenzi yako yasitawaliwe na migogoro. Unatakiwa ujue jinsi ya kuishi kwa upendo na furaha. Amani itawale kwenye uhusiano, hali kadhalika tabia zako zikidhi mahitaji ya katiba ya mapenzi au ndoa yako.Je, unatakiwa uyafanyie nini mapenzi yako au ndoa yako? Muonekano wako uweje mbele ya mwenzi wako? Ukiwa na hasira, ni kitu gani cha kufanya? Inapotokea mpenzi wako ameghadhibika, jambo lipi ufanye liweze kumrudisha kwenye mstari unaotakiwa?
Ndoa inahitaji nini? Kwa nini aliye kwenye ndoa hatakiwi kujiona ana uhuru wa kupitiliza kiasi cha kumuathiri mwenzi wake? Nini wajibu na haki za mtu kwenye mapenzi? Ni kwa namna gani mtindo wa maisha wa bachela, ukitekelezwa na mwanandoa ni sumu?

Hayo na mengine mengi, yanachambuliwa kinagaubaga kwenye katiba ya mapenzi. Mtu sahihi ni yule anayeishi kwa kujiamini, si ambaye anafanya kwa kujaribu, akisubiria matokeo au mapokeo ya mpenzi wake. Mapenzi ni rahisi mno endapo utaheshimu muongozo.
Katiba yenyewe inaundwa na vipengele vingi ambavyo nitavichambua katika wigo mpana ili uweze kuelewa ipasavyo. Inahitaji utulivu na umakini wakati wa kusoma, mwisho utakuwa ni mwenye mafanikio makubwa endapo yaliyomo kwenye maandishi yangu yatakita vilivyo ndani ya ubongo.

UPENDO
Hiki ni kipengele kikuu. Unaweza kukiita kifungu mama ndani ya katiba ya mapenzi. Huwezi kusema upo kwenye uhusiano makini kama upendo haupo katikati. Chukua hatua madhubuti endapo utabaini upendo haupo. Mkatae mwenzi ambaye hakupendi, kinyume chake atakupa mateso mbele ya safari.
Muongozo wa kipengele cha upendo ni kwamba lazima wewe mwenyewe uanze kuwekeza upendo kisha naye akupende. Ni maisha ya ubinafsi kutaraji kupendwa, wakati wewe mwenyewe huoneshi kwa mwenzako. 
Zingatia hili kila siku na wakati wote ili uweze kufaidi matunda mema kwenye uhusiano wako.
Kuna tabaka la watu ambao huishi kwa kusikilizia zaidi. Haitakiwi kutegea, upendo unamaanisha pande mbili zinazovutana. Huyu anatekeleza hili kwa ajili ya mwenzake, hali kadhalika na mwingine anasimama imara kuhakikisha mpenzi wake anafaidi malisho mema ya mapenzi. Hakikisha mpenzi wako hakushindi upendo, onesha unampenda zaidi.
Upendo huyeyusha mengi. Ukiwekeza upendo kwa mwenzi wako, utamfanya nafsi yake iwe na woga. Ni rahisi kushinda vishawishi, kama atakuwa akikaa peke yake anakuwa anajiridhisha kuwa unampenda kwa moyo wako wote. Vinginevyo, anaweza kushawishika na kukusaliti kama tu akili yake itamtuma kuamini kwamba humpendi.

Hivyo basi, hakikisha upendo wako si wa wasiwasi. Mfanye awe na imani, ikabidi imani ya kupitiliza. Utafiti unaonesha kuwa mtu aliyeonesha upendo mkubwa kisha akasaliti kwa tamaa zake, anapobainika na kuachwa hujuta zaidi kuliko yule aliyeona hakukuwa na upendo kwa sababu haoni cha kupoteza.

HOFU
Wengi hawajui hili. Unaweza kuwa na upendo mkubwa kwa mwenzi wako lakini kama huna hofu juu yake, ni sawa na bure. Katika kipengele hiki, nashauri watu kujitenga na maneno yasiyo na faida. Mapenzi siyo tamko la kinywa peke yake, moyoni ndiyo mahali pake. Hii inamaanisha kuwa mapenzi hayatamkwi mdomoni na yakaisha. 

Ni lazima mwili mzima uhusike kivitendo. Mantiki hapo ni kuwa unaweza kusema unapenda lakini kama huna hofu yoyote kwa huyo umpendaye, ni sawa na kupiga gitaa kumtumbuiza mbuzi, kwani hakutakuwa na matokeo mazuri.
Faida ya hofu kwenye uhusiano ni kuwa kila nukta, dakika, saa na siku, utaishi kwa tahadhari. Lile ambalo unajua haliwezi kumpendeza mwenzi wako, hutalifanya, hivyo kufanya maelewano kuwa makubwa zaidi. Husaidia kuepusha migogoro na kuumizana bila sababu za msingi.

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment