Monday 14 January 2013

VIJIMAMBO: JE? WAJUA KUHUSU KABILA LA WAHEHE NA ULAJI WA MAJANI? IJUE ASILI YAKE

VIJIMAMBO
thumbnail JE? WAJUA KUHUSU KABILA LA WAHEHE NA ULAJI WA MAJANI? IJUE ASILI YAKE
Jan 14th 2013, 21:57

Marehemu Chifu Mkwawa enzi za uhai wake 

Na Francis Godwin, Iringa
KABILA la WAHEHE ni kama yalivyo makabila mengi ya kibantu yaliyomo nchini Tanzania, ambao wao walikula majani, mizizi na matunda pori pamoja na vitu ambavyo vilirithiwa vizazi na vizazi vilivyofuata na hatimaye kuwa vyakula vya kawaida kama mizizi, miti, matunda na majani.
Mzizi wa mti wa "MTONO" huliwa ungali bado mchanga ambao huitwa "ISONGI" unaochimbwa wakati wa masika au mahali palipo na unyevunyevu, huliwa kama mtu alavyo muwa kwa kumenya maganda.
Mti wa "AMAKINGILIGITI" huzaa matunda yaliyo na sura kama "golf" matunda haya, radha yake ni kama limao ingawa radha hiyo haijafananishwa kisayansi, lakini hufanana na dawa za vitamini "B Complex" majani yake huliwa na mbuzi mwitu (aitwae INGULUGULU kwa lugha ya kihehe) na mbegu zake huliwa pia.
"MUTOWO" huzaa matunda wakati wakiangazi ambapo matunda yake huwa na nyuzi nyuzi wakati wa kutafuna mithili ya mtu atafunaye bigijii na zikitafunwa hutoa utomvu mzito wenye sukari nyingi, hazimezi kwa sababu zinawasha sana kwenye koromeo na huweza kuleta kikohozi cha muda mrefu.


Aidha mtu akila huweza kupatwa na hamu ya kiu ya kunywa maji hasa akiwa na kazi ngumu na pia huweza kuandaliwa kwa kuchemshwa na kudumu kwa muda wa miezi sita bila kuoza. 
Matunda "MUNYWEWA" huwa katika ganda gumu ambalo ndani yake kuna maji matamu yanayonywewa na yanapunguza kiu yanafanana kabisa na mti wa MTANGADASI ambao hauna maji ila una nyama nzito ambayo ni chakula kizuri cha nyani na ngedere.
"AMAMBEDEE" hujulikana kama tango, mmea huu hutambaa kama mmea wa maboga hupendelea kuota zaidi kwenye mbolea ya samadi na walaji wakuu ni wenyeji wa mkoa wa Iringa na pia huliwa na wanyamapori hada digidigi.
"MAGUHU" mti wake ni mwepesi sana ukifananisha na MSONOBALI (CYPRESS) hustawi sana katika mbuga za mwinuko.Wahehe huita "MUWUBAMBA" ambao hauwezi kutumika kama kuna nishati ya kupikia kwa sababu ya wepesi wake huwaka mfano wa karatasi, matunda yake huwa mekundu na ndani yake huwa na uji wa rangi ya njano na ndiyo huliwa, linazo mbegu mbili zinazofanana sana ni laini lakini haziliwi.
Upo mti mwingine ujulikanao kama "MUFUDU" ambao huzaa matunda ya MUFUDU ambayo huliwa baada ya kukomaa lakini yakiwa hayajakomaa yanakuwa ya kijani huwezi kula machungu, matunda haya yana rangi nyeusi tii mithili ya kiwi, nyama yake huwa nyeusi pia na mbegu yake hailiwi hutupwa.

Haifahamiki pia ni kwa nini Wahehe walio weusi tii hufananishwa na MUFUDU.
Inaelezwa kuwa Mtwa GUNGIHAKA TOVELA PATELI mdogo wa Mtwa MKWAWA alikuwa mweusi tii lakini weusi wake ulifananishwa na weusi wa NYATI wakimwita "WUTITU WA MBOGO" na "MUFUDU" wakimananisha ni mweusi kama NYATI na MUFUDU.
"MUSAULA" ni mti unaofanana na miti ya MINYWEWA, MUTANGADASI, MUTUNDWA na MUGUHU ambao huota nyanda zilizoinuka na hukomaa kiangazi tu kwa hiyo ni tunda la msimu kati ya mwezi Mei, Juni na Julai ni chakula cha NYANI pia huliwa na watoto wadogo zaidi.
"MUSANSAWUKI" ni aina ya majani ambayo huota msimu wa masika tu, huzaa matunda yenye miba mingi sana. Matunda hayo hutoa maua mengi yenye rangi nyekundu na haya maua mekundu huwa na utomvu ambao ukifyonza ni mtamu. Utomvu huo huitwa Wununu ambao pia huliwa na vipepeo na nyuki na watoto (binadamu).
Mizizi, majani na matunda machache yaliyoainishwa hapo juu yalikuwa na pengine bado yanaliwa na Wahehe kutoka siku za kale. Nia na makusudi ya kuandika makala haya ni kukielimisha kizazi cha sasa kuwa wazazi wao walikula vyakula hivyo vya porini ambayo vilisaidia kushinda magonjwa mbalimbali mwilini kwa sababu vilitoa kiwango madhubuti mwilini.
Vijana wengi wa siku hizi ambao hawataki au hawajui vyakula vya porini vipo, wamekuwa kivutio kikubwa kwa magonjwa mbalimbali kwa sababu ya kukosa kinga ya ziada.

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment