Sunday 21 April 2013

VIJIMAMBO: MARY KATOBESI: Nilipewa zawadi ya Sh500 na Nyerere

VIJIMAMBO
MARY KATOBESI: Nilipewa zawadi ya Sh500 na Nyerere
Apr 21st 2013, 23:49




"Mimi ni mmoja wa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia, kutokana na mila na desturi, baba alinibagua mimi na wenzangu wawili, nikaishia kidato cha pili."
Hiyo ni sehemu ya maelezo ya Mary Fred Katobesi, mzaliwa wa Old Moshi mkoani Kilimanjaro, miaka 53 iliyopita.
Mama Katobesi ambaye sasa ni Mshauri wa Kisheria, Mwalimu wa Ujasiriamali, akiwa pia ni Katibu wa Ukonga Vikoba Saccos iliyopo Jimbo la Ukonga, mkoani Dar es Salaam anasema kuwa katika familia ya baba yake Mzee Manga walizaliwa watoto sita, watatu wavulana na watatu wengine, wasichana.
Anaeleza kuwa alisoma Shule ya Sekondari Natiro iliyopo Mbokomu Moshi Vijijini na alipofika kidato cha pili, baba yake ambaye ni Mkandarasi wa Ujenzi alikataa kumlipia ada akieleza kuwa watoto wa kike hawastahili kusoma kwa kuwa hawana faida kwa jamii, hali ambayo iliwakuta pia wenzake wawili aliozaliwa nao.
"Baada ya hapo binamu yangu alinichukua na kunileta jijini Dar  es Salaam kwa ahadi ya kunisomesha uhazili kwa wakati huo, lakini nilipofika kwake nikaishia kufanya kazi za ndani ," anasimulia Mama Katobesi.
Anaongeza kuwa baadaye alichukuliwa na kaka aliyemsaidia kupata kazi katika kiwanda kilichojulikana kama Tanzania Outoparts, ambapo alijifunza na kufanya kazi ya kutengeneza 'filter' za magari ya diseli.Anabainisha kuwa wakati akifanya kazi katika kiwanda hicho, siku moja mwaka 1977 Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alitembelea kiwanda hicho.
"Katika ziara hiyo, uongozi wa kiwanda ulimpa Mwalimu Nyerere zawadi ya Sh500 naye alinipa mimi akaagiza niendelezwe," anasimulia.
Anafafanua :"Lakini, Mkurugenzi wa Tanzania Outoparts akataka niwe mke wake mdogo ndipo aniendeleze, kunijengea nyumba na kunirithisha mali zake. Mimi nikakataa na kutoroka."
Anaongeza kuwa baada ya tukio hilo, mkurugenzi huyo aliyekuwa wa jamii ya Singasinga aliogopa na kuanza kunitafuta bila mafanikio, baadaye naye alitoroka nchini na kutelekeza kiwanda, kikafa.
"Ile Sh500 niliyopewa na Nyerere nikanunua samani za kuanzia maisha, lakini kaka yangu Lucas Manga alinipeleka VEATA nikasomea ushonaji, muda mfupi baadaye nikaolewa, hiyo ilikuwa mwaka 1980, " anasema. Anaeleza kuwa alipata msukumo akajiunga na mafunzo ya utengezaji batiki yaliyotolewa na wamisionari waliokuja nchini kupitia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambao walianzasha vikundi vya kuendeleza jamii wakishirikiana na VETA, kupewa mitaji na baadaye alikuwa mwalimu wa utengenezaji batiki.
"Nilianza biashara ya batiki huku nikifundisha wanawake wenzangu, wengi kwa vikundi. Batiki zikaenda hata mikoani, bahati mbaya wanawake wenzangu wengi wakafariki kipindi hicho kwa magonjwa ya kisasa, nikaanza kulea yatima," anasema na kuongeza:
"Mwaka 1999-2000 nikaenda kusomea Vicoba kwa miezi mitatu, nikahamasisha watu mitaani tukaanzisha ujirani mwema wa kusaidiana nikiwa na wenzangu 15, tukasajili umoja wetu na sasa ninalea watoto yatima 340, mmoja tayari anafanya kazi ATCL, mmoja mwalimu na mwingine mfanyabiashara."
Akizungumzia nafasi yake ya Ukatibu wa Ukonga Vicoba Saccos, Mama Katobesi anasema kuwa Saccos hiyo imeanzishwa kwa kushirikisha jamii ambapo tayari ina wastani wa wanachama 2010, wakiwa na mpango wa hivi karibuni kufanya harambee, wakitarajia kukusanya Sh600 milioni, ili kuwakopesha wajasiriamali na wananchi wengine mara nne ya akiba ya mwanachama ili kuinua uchumi na maisha ya wananchi wa Ukonga.
Saccos hiyo ipo chini ya ulezi wa Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Eugen Mwaiposa."Kiwango cha riba ni tofauti na Saccos nyingine,watatamka wanachama wenyewe, wana Ukonga tuiinue hii Saccos, tuwe waaminifu, ituinue kiuchumi, tukikopa turejeshe," anasema.
Mama Katobesi pia amewakusanya wajane wapatao 50 na kuwapa nguvu ya kuichumi ili kujikimu kimaisha kwa kuanzisha miradi ya bustani, uuzaji wa sambusa na maandazi, ambao sasa wana uhakika wa mlo wa siku na familia zao.
Mwaka 2010 alipata mafunzo ya usaidizi wa sheria kupitia Chama cha Wanasheria Wanawake (WLAC) na baadaye kupitia Tanzania Women and Child Walfare(TWCWC) na kuweza kusaidia wengi wanaonyayasika, wanaonyayasika kijinsia hata watoto kwa kuwapa ushauri wa kisheria hata kuwapeleka katika mashirika ya msaada wa kisheria.
Anasema kuwa kuptia mafunzo hayo amebaini kuwepo kwa tatizo kubwa la unyayasaji wa kijinsia, baadhi ya wanaume kuoa na kuacha.
"Ukonga hakuna kuoa, ni mimba na kuacha kisha wanaume wanahama na kuacha wanawake. Unyayasaji ni mkubwa hata watoto wenye wazazi, bado wananyayaswa," anaeleza mama Katobesi.
Akitoa ujumbe wake kwa jamii anasema kuwa: "Sikati tamaa ya kueleimisha jamii Ukonga na Tanzania kwa jumla. Nawaomba watoa ruzuku wakumbuke maeneo ya mijini, wasikimbilie vijijini pekee, kwani matatizo ya vijijini mengi yanahamia  mijini."
Mwananchi

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment