Friday 18 January 2013

VIJIMAMBO: Mkuu wa Itifaki wa Marekani amuaga Balozi Maajar

VIJIMAMBO
thumbnail Mkuu wa Itifaki wa Marekani amuaga Balozi Maajar
Jan 18th 2013, 22:49

Balozi Capricia Penavic Marshall, Mkuu wa Itifaki Marekani, akitoa maelezo kuhusu utendaji kazi wa Balozi Maajar wakati wa hafla fupi aliyoiandaa ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani leo Ijumaa tarehe 18, Machi 2013 kwa heshima ya Balozi Mwanaidi na Bw. Shariff Maajar. 
Mkuu wa Itifaki wa Marekani Balozi Marshall leo amesema Balozi Mwanaidi Maajar amefanya kazi kubwa ya kudumisha mahusiano baina ya Marekani na Tanzania na Jumuiya ya Wanadiplomasia hapa Washington DC watamkumbuka kwa hilo.
Aliyasema hayo kwenye hafla fupi ya chai ya asubuhi aliyoiandaa kwa heshima ya Balozi Mwanaidi Maajar na Bw. Shariff Maajar wanaotarajia kurejea nchini Tanzania baada ya kumaliza muda wa uwakilishi nchini Marekani.
Miongoni mwa mambo ambayo Balozi Marshall ameyataja kuhusu Balozi Maajar ni kile alichokiita uwezo wake mkubwa wa kazi ya uwakilishi akitoa mfano wa Balozi Maajar kuuliza maswali yanayohusu mahusiano baina ya Marekani na Tanzania kwenye ziara zote zilizoandaliwa na mkuu huyo wa itifaki kwenye majimbo mbalimbali ya Marekani. 
"Kila mara tunapokuwa safarini, sehemu ya maswali ikifika, Balozi Maajar yeye huwa wa kwanza kwenye kipaza sauti na kuuliza maswali au kuchangia mazungumzo ili kuhakikisha mahusiano ya nchi zetu mbili yanakua" alisema Balozi Marshall.

Alichukua pia nafasi ya kusoma waraka ulioandikwa na Mhe. HIllary Rodham Clinton, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akimtakia Balozi Maajar kila la kheri na mafanikio mengi mara arudipo Tanzania. 

Balozi Marshall alisisita amefurahi sana kupata fursa ya kufanya kazi na Balozi Maajar na japokuwa anarudi Tanzania, lakini msingi wa mahusiano baina ya nchi hizi mbili utaendelea kudumu daima, na yeye binafsi anajua anarafiki Tanzania. 

Kwa upande wake Mhe. Maajar alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kuendeleza mahusiano baina ya nchi mbili. Pia aliishukuru serikali ya Marekani kwa programu mbalimbali zinazoendelea Tanzania zikiwemo mpango wa kutokomeza malaria, UKIMWI, lishe bora kwa mama na mtoto na kilimo. 

Alitangaza kuwa Mkataba wa pili wa Milenia au Millenium Challenge Compact umepitishwa huu ukiwa ushahidi tosha wa ushirikiano baina ya Marekani na Tanzania ambapo Watanzania wengi watanufaika nao hususan kwenye upande wa kuboresha miundo mbinu, kilimo, elimu na afya.

Akinukuu maneno ya Rais Kikwete ambaye amemuwakilisha nchini Marekani kwa miaka miwili, Balozi Maajar amesema, "Tunathamini sana uhusiano wetu na watu wa Marekani, hivyo nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuhakikisha mahusiano yetu yanakua". 

Balozi Maajar alimuomba Balozi Marshall afikishe salamu zake za shukrani kwa Mhe. Hillary Clinton kwa jitihada zake kubwa za kuitangaza sera ya Mambo ya Nje ya Marekani huku akitoka kipaumbele kwenye masuala ya maendeleo ya wanawake. 

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali hususan za kiafrika na baadhi ya wafanyakazi wa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na marafiki, ilifanyika kwenye chumba cha James Monroe, ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyopo mtaa wa C, mjini Washington D.C. 

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment