Sunday 13 January 2013

VIJIMAMBO: Koti la muungano halitufai- Maalim Seif

VIJIMAMBO
thumbnail Koti la muungano halitufai- Maalim Seif
Jan 13th 2013, 19:48

Salma said, zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad leo amekutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kutoa maoni yake binafsi kuhusiana na mtazamo wake juu ya katiba mpya ya Tanzania ambapo amesema koti la Muungano linawabana wazanzibari kwa sasa.

"Koti la Muungano sasa linatubana sana, na kwamba tunahitaji kushona koti jipya kulingana na hali zetu za sasa", alisema Maalim Seif mbele ya tume ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Maalim Seif ambaye amekuwa kiongozi wa Kwanza mashuhuri kukutana na tume hiyo katika utaratibu wa ukusanyaji wa maoni amesema katika kipindi cha miaka 49 ya Muungano bado hakujakuwa na nia njema ya kutatua kero za Muungano, hali inayopelekea kuongezeka kwa kero hizo na kuleta usumbufu kwa wananchi hasa wa Zanzibar.

Amesema kutokana na hali hiyo ni vyema muundo wa Muungano ukaangaliwa upya, na kusisitiza msimamo wake wa kuwepo Muungano wa Mkataba ambapo kila nchi itakuwa na mamlaka yake kamili ndani na nje ya nchi na baadae kushirikiana katika mambo ya msingi ambayo yataamuliwa na pande hizo mbili.

Maalim Seif ambaye ametoa maoni hayo nyumbani kwake Mbweni Zanzibar amefahamisha kuwa muundo wa Muungano wa serikali mbili uliopo sasa hauwezi kutatua kero za Muungano baada ya kuwepo kwake kwa kipindi cha miaka 49 bila ya kuonyesha mafanikio ya kuridhisha ya kutatua kero hizo.

Amesema katika kipindi hicho tume na kamati kadhaa zimeundwa katika kushughulikia kero za Muungano, lakini mafanikio yake ni madogo, hali inayotia wasiwasi wa kuongezeka kwa kero hizo badala ya kutatuliwa.

Amefahamisha kuwa Zanzibar imekuwa muathirika mkubwa wa Muungano uliopo hasa katika Nyanja za kiuchumi na siasa, baada mshirika wake wa Muungano (Tanganyika) kutoweka, na kutumika jina la Tanzania kwa maslahi ya upande mmoja wa Muungano.


Maalim Seif anatarajiwa kukutana na waandishi wa habari hapo kesho katika hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar, ili kuyatolea ufafanuzi maoni hayo na kuyaweka bayana kwa wananchi wote maelezo yake aliyoyatoa katika tume ya mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment