Saturday 2 March 2013

VIJIMAMBO: SULUHU HAIPATIKANI KWA KUTOKA NJE YA NDOA

VIJIMAMBO
thumbnail SULUHU HAIPATIKANI KWA KUTOKA NJE YA NDOA
Mar 2nd 2013, 08:33

NAAM tumekutana tena kwenye kona yetu ya Mapenzi na Uhusiano ili kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku. Asilimia kubwa ya maisha yetu yametawaliwa na mapenzi. Nasema uongo?
Nitakuwa si muungwana kuanza mada mara moja bila kujuliana hali, binafsi sijambo, sijui mwenzangu u hali gani tangu tuachane wiki iliyopita! 

Naamini kwa uwezo wa Mungu u mzima, kama ni mgonjwa basi Mungu akupe wepesi wa kupona haraka na kama kuna aliyetangulia mbele ya haki, apewe mapokezi mema ili apumzike kwa amani.
Leo kuna kitu kimoja kimenivuta kukaa mbele ya compyuta na kuyaandika haya, kama kichwa cha habari hapo juu kinavyojieleza.
Waswahili wana usemi wao kuwa, usipoziba ufa utajenga ukuta, huo usemi ni kweli kabisa, baada ya kushuhudia tukio moja ambalo nina imani lipo ndani ya nyumba zetu.
Nasema hivi baada ya juzi kumsikiliza mwanaume mmoja akilalamika kitendo cha mkewe kukataa kumpa haki yake ya ndoa, baada ya kukorofishana kwa jambo lisilo na maana yoyote. 

Bwana yule nilimsikia akimlalamikia rafiki yake kuwa mkewe amekuwa na tabia za kumnunia bila sababu, hata kama ni kitu cha kuzungumza na kuelewana yeye hununa hadi kufikia kupeana migongo kitandani, kila mtu kujifunika shuka lake.

Jamaa alimueleza rafiki yake kuwa kutokana na tabia za mkewe, ameamua kutafuta mtu wa nje ambaye amekuwa akimliwaza kila siku. Kwa kweli kauli ile ndiyo iliyonifanya niandike makala haya.

Ni ukweli usiopingika kuwa wanaume wengi sasa hivi wamejikuta wakitafuta suluhu ya matatizo ya ndoa zao kwa kutoka nje ya ndoa. Hii imefanya nyumba ndogo ziwe nyingi kila kukicha, kutokana na baadhi ya watu kushindwa kuelewa maadili ya ndoa yanasemaje pindi wanapokorofishana na wenza wao.

Hilo si kwa wanawake tu, hata baadhi ya wanaume huwanyima haki za ndoa wake zao pengine kutokana na kupata mwanamke wa nje. Kwa vile mkewe naye ana hamu zake na pa kuzitoa hana, kwa wenye mioyo dhaifu hutafuta mtu wa nje ili kukidhi haja. Nataka kusema kuwa, kutoka nje ya ndoa si ufumbuzi wa tatizo, bali ni kuongeza ufa sehemu yenye mpasuko ambayo itaiangusha nyumba kabisa.

Siku zote suluhu ya ndoa haipatikani kwa mtu kwenda kutafuta mpenzi nje, bali kukaa chini na mwenzako ili kumaliza tofauti zilizojitokeza.
Kwa wanandoa wenye busara, linapotokea tatizo hukaa chini na kuelewana, wala hakuna atakayetaka kumkomoa mwenzake kwa kumnyima haki yake. Unamnyima haki yake wakati wewe ndiye mkewe au mumewe aliyekuchagua, unataka akaitafute wapi? 

Unamlazimisha awe na nyumba ndogo au bwana wa pembeni. Thamani ya kitu ione wakati unayo, siku zote kibaya unacho lakini kikikutoka si chako tena, hapo ndipo utakapoijua thamani yake.
Mtu kumnyima haki ya ndoa mwenza wake si kutatua tatizo, bali ni kuongeza ukubwa wake na kutoka nje ya ndoa si kutatua tatizo, bali ni kuzidi kuibomoa nyumba.

Siku nyumba yenu itakapoporomoka muanguko wake ni mbaya, mwenzako akirudi na magonjwa ndani, nani wa kumlaumu? Huoni wewe ndiye chanzo? Siku zote kunapotokea tatizo tafuteni suluhu ya kutatua bila kumuathiri mtu yeyote. Oneaneni huruma, hakika hakuna atakayemuumiza mwenzake.
GPL

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment