Friday 29 March 2013

VIJIMAMBO: Marashi,sabuni;Onyo kwako mwanamke

VIJIMAMBO
Marashi,sabuni;Onyo kwako mwanamke
Mar 30th 2013, 01:38

Sabuni au mafuta yenye kemikali  huchubua  ngozi laini ya uke na ni rahisi vimelea vya magonjwa kuenea kwa urahisi.
Wanawake ni miongoni mwa wanajamii wengi wanaopenda kutumia marashi na vitu vingine kama sabuni zenye kemikali kwa ajili ya kujirembesha.
Pia, wanawake wamekuwa wakipenda usafi wao binafsi, wakitumia vitu  ambavyo baadhi yake ni hatari.
Wapo baadhi ya wanawake wanaopenda kusafisha sehemu zao za siri kwa kutumia sabuni zenye kemikali, marashi (pafyumu) au kupaka mafuta.
Kwa maelezo ya wataalam, hao wapo hatarini kupata magonjwa ya zinaa au ya kuambukiza.
Watafiti katika Chuo Kikuu cha California, Marekani wanasema sabuni ngumu au hata za maji, pafyumu (deodorant) zinaharibu tishu muhimu zilizomo ndani kabisa ya uke na kumweka mhusika katika hatari ya kupata malengelenge, fangasi  na hata Ukimwi.
Aidha, sabuni au dawa zinazouzwa na wafanyabiashara zikitangaza kuboresha uke au kuondoa harufu kwenye sehemu hizo nyeti nazo zimeelezwa kuwa na madhara.
 Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Cyriel Massawe anasema sabuni au mafuta yenye kemikali  huchubua  ngozi laini ya uke na ni rahisi vimelea vya magonjwa kuenea kwa urahisi.
Dk Massawe anasema michubuko hiyo ambayo si rahisi kuonekana kwa macho ndicho chanzo cha kuingia kwa maradhi ya kuambukiza.
"Hamna haja ya kuweka kemikali, au pafyumu ukeni. Hizo sehemu zinahitaji kuoshwa vizuri kwa maji," anasema Dk Massawe.
Anasema kemikali inapoingia ukeni inavuruga hali ya kawaida na asidi inayolinda sehemu hizo.
Anaongeza  kuwa ni vyema wanawake wakaelimishwa kuhusu matumizi ya  bidhaa zinazodaiwa kuweka harufu nzuri  katika sehemu zao za siri, kurudisha bikira au mafuta ya kulainisha uke.
Naye Daktari Bingwa wa Kitengo cha Patholojia MNH, Henry Mwakyoma anasema wanawake wanaofanya usafi sehemu zao za siri kwa kutumia bidhaa au baadhi ya vifaa visivyofaa kutumiwa ukeni huweza kupata saratani ya shingo ya uzazi.
Dk Mwakyoma aliyewahi kufanya utafiti kuhusu saratani ya shingo ya kizazi nchini anasema, bidhaa zenye kemikali ya 'coal tar,' ambazo mara nyingine huwekwa kwenye sabuni ama manukato na kutumiwa ukeni na wanawake huweza kuchochea saratani hiyo.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Joelle Brown, alisema upo ushahidi wa kutosha kuwa kutumia sabuni za kuogea za maji au ngumu katika sehemu za siri za ndani za mwanamke kunaharibu uwiano wa bakteria na kusababisha bakteria kuzalishwa kwa wingi na kumweka mwanamke katika hatari ya maradhi ya  zinaa ya kuambukiza.
Timu ya Dk Brown iliwafanyia utafiti wanawake 141 ambao walikubali kujibu maswali kuhusu sabuni wanazotumia na kisha walikwenda kupimwa maabara iwapo wamepata maradhi ya kuambukiza ukeni.
Watafiti walibaini kuwa asilimia 66 ya wanawake waliokuwa wakitumia mafuta na sabuni kusafisha sehemu za siri walikuwa wamepata maradhi ya kuambukiza.
Bidhaa za  uke zilizoonekana kutumiwa zaidi na wanawake ni mafuta ya kulainisha uke wakati wa tendo la ndoa, ambapo asilimia 70 ya wanawake walionekana kutumia.
Asilimia 17 waliripotiwa kutumia mafuta mazito ya kujipaka(petroleum jelly) na wengine asilimia 13 walitumia mafuta ya kawaida.
Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa wanawake waliotumia mafuta kama vile vaseline kujipaka katika sehemu zao za siri walipata maambukizi ya bakteria na fangasi kwa urahisi.
Asilimia 44 ya wanawake waliotumia mafuta kulainisha uke na pafyumu walionekana na maambukizi ya fangasi aina ya candida.
Wataalamu hao wa afya walisema uke ni sehemu inayoishi bakteria wabaya na wazuri ambao huzalisha asidi maalumu inayolinda eneo hilo lisipate maambukizi na virusi.
Madaktari hao walishauri  wanawake kutoosha sehemu za ndani kabisa za uke kwa bidhaa zozote, au kuingiza mafuta ya aina yoyote kwa sababu kufanya hivyo kutaharibu uwiano wa bakteria wabaya na wazuri.
Mwenyekiti wa Kituo cha Magonjwa ya Wanawake cha Mtakatifu Elizabeth, Michael Zinaman alisema hata matumizi ya pafyumu sehemu za siri si mazuri.
Mary Marnach, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika Kliniki ya Mayo, Minnesota pia kule Marekani anasema  mafuta au vimiminika vinavyotumika ukeni huwa na glycerini ambayo baadaye hubadilika na kuwa sukari hivyo kuzalisha fangasi na bakteria wabaya.
"Pafyumu husababisha mabadiliko katika uke au kuongeza asidi ndani yake" anasema Dk Marnach.
Anaongeza kuwa asidi ya kawaida katika sehemu hiyo Ph nne au tano. Iwapo asidi nyingine itaingia katika eneo hili inabadilisha na kusababisha  matatizo wala si faida.
Anaeleza: "Pafyumu huweka harufu nzuri sawa, lakini kwa  dakika chache na baada ya hapo husababisha harufu mbaya kwa sababu inazalisha bakteria wengine."
Mtaalamu huyo anaongeza kuwa matumizi ya muda mrefu ya pafyumu, poda, mafuta au sabuni ndani ya sehemu hiyo nyeti na laini husababisha  chembechembe kuingia ndani  ya mfumo wa uzazi wa mwanamke na kusababisha madhara makubwa.
"Kama mwanamke ana afya, anajisafisha kwa maji ya kawaida kila mara na kubadilisha nguo za ndani, hana haja ya kujipuliza pafyumu au kujisafisha kwa sabuni zenye kemikali katika eneo hilo," anasema Dk Manarch.
Mwananchi

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions

No comments:

Post a Comment