MUNGU kwa kunijaalia fursa hii ya kuzungumza nanyi wapenzi wasomaji wa safu hii ya Mashamsham. Natumaini muwazima na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida.
Ndugu zangu, kwa wale walio katika mapenzi matamu na ya kweli watakubaliana na mimi kuwa mapenzi yenye amani na masikilizano ni kama 'kaparadiso' kadogo ndani ya ulimwengu huu mkubwa uliojaa vituko!
Wakati mwingine unaweza hata kujikuta umeshiba bila kula, eti kwa sababu tu umemuona mpenzio au kuwa naye karibu yaani yeye kwako ndo' mambo yote, yeye ndiyo kila kitu! Raha ilioje!
Lakini sasa, wakati baadhi ya watu wakiwa katika maisha ya furaha kutokana na kujaaliwa kuwa na wapenzi wenye mapenzi ya dhati, wapo ambao wanateseka kwa kujiingiza kwenye mapenzi ya kisanii.
Kabla sijaingia ndani zaidi kuzungumzia hili la mapenzi ya kisanii, ni vizuri kama tutajiuliza kwa pamoja maana ya mapenzi kama tulivyoletewa na Mungu! Tunaposema mapenzi huwa tunamaanisha nini hasa?
Katika hili najua kila mmoja anaweza kuwa na maana yake lakini kwa haraka haraka naweza kuyatafsiri mapenzi kama hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine. Hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na za dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo.
Hii ndiyo maana ya haraka haraka ya mapenzi. Kwamba unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyetokea kumpenda hupaswi kuwa na mtu mwingine kwa kuwa, kwa kufanya hivyo utakuwa huutendei haki moyo wako.
Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imechakachuliwa kabisa, imepotoshwa na kubadilishwa huku kila mmoja akiyachukulia kama anavyoona yeye na kujiona yuko sahihi. Mapenzi ya siku hizi yamejaa ujanjaujanja mwingi, wengi wakiwa ni wasanii wanaojifanyisha ilimradi wapate kile wanachokihitaji.
Tunajua matatizo mengi yanaweza kutukumba iwapo tutakuwa si waaminifu kwa wapenzi wetu, tunajua kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ni kujitafutia matatizo ambayo mwisho wa siku tunaweza kujikuta tunajuta na kutoa machozi lakini cha ajabu bado tunaendelea kufanya hivyo.
Tunaelewa wazi inavyouma kusikia mpenzi wako ana mtu mwingine lakini sisi mbona tunawafanyia wenzetu hivyo? Hatuoni kwamba kwa kufanya hivyo tunakwenda kinyume kabisa na maana halisi ya mapenzi?
Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi kibao huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya.
Wapo wake za watu ambao wanapatiwa kila kitu na waume zao lakini bado eti wanatafuta 'vijiwanaume' vya pembeni na baadaye hao hao wakikutana na waume zao wanajifanya wapole, wanyenyekevu na wenye mapenzi ya dhati, wizi mtupu!
Nasema wizi mtupu kwa kuwa wanaofanya ujanjaujanja kwa wapenzi wao hawana mapenzi ya dhati, ukichunguza utabaini wamependea pesa au mali na matokeo yake sasa ni kujifanyisha kuwa wanapenda kumbe hamna lolote.
Huko nyuma tulikuwa tukiyaona haya kwa wapenzi wa kawaida lakini sasa hivi huwezi kuamini hata ndoa zimekuwa za kisanii na ndiyo maana nyingi hazidumu.
Wanaoana leo na baada ya mwaka mmoja unashangaa mwanamke anaanza visa na akishatamkiwa suala la kuachwa utamsikia akisema, wagawane mali. Yaani hicho ndicho alichokifuata lakini mapenzi hakuna.
Hawa ndiyo wanaotumia pesa za waume/wake zao kusalitia. Mke anachukua pesa za mume anazipeleka kwa 'kiserengeti boy' chake huku baadhi ya wanaume nao wakifanya vivyo hivyo.
Kimsingi huu si wakati wa kufanyiwa usanii katika mapenzi, kinachotakiwa ni kuwa makini na yule ambaye umetokea kumpenda na kufanya utafiti kama na yeye anakupenda. Kamwe usiwe bwege na ukakubali kuingia kwa mtu kichwakichwa ambaye anaweza akajifanya naye anakupenda kumbe kaona pochi yako imenona.
Niishie hapo kwa leo nikiamini utakuwa umajifunza kitu.
GPL
No comments:
Post a Comment